Ijumaa, 3 Oktoba 2014

WAKULIMA WANAWAKE WA MANANASI BAGAMOYO KUKAUSHA MANANASI KISASA KWA KUTUMIA JUA 

Wakulima wanawake wa mananasi kutoka katika kata za Kiwangwa na Fukayosi wilayani Bagamoyo wanatarajia kuanza kukausha mananasi kwa kutumia makaushio ya kisasa yanayotumia jua ambayo yamejengwa katika vijiji vya Kiwangwa kwa kata ya Kiwangwa na Mwavi kwa kata ya Fukayosi. Wanawake hao amabo wanaunda umoja unaoitwa UMOJA WA KUFUTA UMASKINI KATA YA KIWANGWA NA FUKAYOSI (UFUMA-KIFU) wamefanikiwa kupata makaushio hayo chini ya mradi wa KUONGEZA THAMANI YA ZAO LA NANASI KWA WAKULIMA WANAWAKE wilayani Bagamoyo, mradi unaofadhiliwa na kampuni ya FARM AFRICA ya nchini Uingereza na kuendeshwa na kampuni ya kitanzania ya DORT AFRICA yenye ofisi zake jijini Dar Es Salaam. 

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kampuni ya DORT AFRICA, Assumpta Nalitolela makaushio hayo yaliyojengwa kwa gharama ya karibu shilingi milioni kumi na saba (17,000,000) kila moja yatasaidia katika uongezaji wa thamani ya zao la nanasi na hivyo kuongeza kipato kwa wanawake hao. Amebainisha kuwa kwa kuwa lengo la mradi huo ulioanza toka mwaka 2012 mi kuongeza kipato cha wanajamii, hivyo wameona kwa kukausha mananasi kwa kutumia jua maana yake ni kwamba sasa wataweza kuuza mananasi mabichi na yaliyokaushwa, na hii itaongeza kipato kwani sasa mkulima atakuwa na masoko mawili.

Kaushio la matunda linalotumia jua katika kijiji cha Kiwangwa



Naye mwenyekiti wa UFUMA-KIFU bi Farida Mrisho amesema wanategemea kuanza kukausha rasmi msimu huu wa mavuno ambao uko karibu kwani mananasi yameshaanza kuiva mashambani. Ameongeza kuwa kwa sasa bado wako kwenye mchakato wa kupata vibali kutoka TBS ili kuhakikisha wanauza bidhaa zenye ubora unaokubalika. 

Ingawa kuna njia nyingi za ukaushaji wa mboga na matunda lakini njia ya kutumia jua imekuwa ni rahisi zaidi kwani licha ya kuwa haiharibu mazingira lakini pia haihitaji nishati nyingine ya ziada kama vile umeme amabo ni gharama na si wa uhakika kwa nchi kama Tanzania.

Viongozi wa UFUMA-KIFU, kutoka kushoto Makamu Mwenyekiti Mtoro Idd, Mwenyekiti Farida Mrisho na Katibu Mwanahawa Mfikirwa

Hakuna maoni: