CHANGAMOTO YA UHABA WA MAJI NA KILIMO CHA MBOGA MBOGA DAR ES SALAAM
Tatizo la upatikanaji wa maji katika jiji la Dar Es Salaam limekuwa sugu sasa na kuwa kero kwa wakazi wengi wa jiji hili kubwa kuliko yote nchini. Wakati imekuwa ni shida kupata maji kwa matumizi muhimu ya kila siku kama vile kupikia, kunywa na kufanya usafi hali hii imekuwa kikwazo kikubwa kwa ukulima wa bustani za mboga mboga kwenye jiji hili lenye takribani watu milioni tano. kwa sababu kilimo cha mboga kinahitaji maji mengi kwa ajili ya umwagiliaji hivyo tatizo hili la maji limefanya watu wengi kushindwa kujilimia mboga wenyewe na kutegemea kununua kwa wauzaji.
![]() |
Maji yanayotumika kumwagilia bustani za mboga eneo la Mbezi Mwisho |
Na kwa wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha mboga mboga kilio kimekuwa ni hicho hicho cha ukosefu wa maji ya kumwagilia. Hali hii imepelekea watu kumwagilia kwa kutumia maji machafu yanayotiririka kwenye mifereji au yaliyotuama pembezoni mwa bustani zao hali ambayo imefanya watu wengi kutokuwa na imani na usalama wa mboga hizo. Abdallah Said ni mkulima wa eneo la mbezi mwisho anayelima mchicha, chinese na aina nyingine ya mboga za majani, anasema wanalazimika kumwagilia kwa kutumia maji machafu kwa sababu ndio yanayopatikana hivyo hawana njia nyingine ya kufanya. Anaongeza kuwa ni kweli kuna baadhi ya watu ambao hawapendi kula mboga za majani kwa sababu ya maji machafu wanayotumia kumwagilia. Bwana Said anasema hali hii imefanya kutokuwa na wateja wengi na hivyo kuwa ngumu kwa wao kupata kipato cha kutosha kwa ajili ya kujikwamua na umaskini.
![]() |
Bustani ya Mchicha |
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa jiji hili walioongea na nurumpya wameonesha wasiwasi juu ya afya zo kutokana na kula mboga zinazolimwa katika mazingira machafu kama ilivyo maeneo mengi ya Dar Es Salaam. Wengi wa waliohojiwa wamesema wanakula kwa sababu tu hakuna namna nyingine huku wakimwomba Mungu awanusuru na madhara wanayoweza kuyapata kutokana na kula mboga zinazomwagiliwa na maji taka. Bi Sofia Mushi mkazi wa Kimara, Dar es Salaam amesema yeye kwa upande wake hana jinsi kwa sababu anajua mboga za majani ni muhimu kwa afya ya familia yake hivyo inambidi tu anunue bila kupenda. Lakini wakati bi Mushi akibainisha hayo mkazi mwingine Mwanaisha Shabani amesema yeye hununua mboga za maji kutokana na unafuu wa bei ukilinganisha na bei ya mboga nyingine kama nyama hivi. Anasema swala la kupata au kutokupata madhara kutokana na kula mboga hizo anamuachia Mungu wake.
Na japokuwa kuna wakati wakazi wengi wa Dar Es Salaam walipigia kelele swala la mboga za majani kumwagiliwa kwa kutumia maji taka bado imeoneakana hakuna ufumbuzi wa haraka wa tatizo lenyewe. kwani kama wanavyolalamika wakulima wenyewe tatizo kubwa ni upatikanaji wa maji, na sehemu kubwa zinazolimwa mboga hizi ni kwenye mabonde ambapo ndio kunapatikana maji ya mito. Na bahati mbaya sana ni kwamba mito yote ya jiji hili imejaa uchafu kupitiliza
![]() |
Wafanyabiashara wa mboga za majani wakiwa sokoni |
Kwa upande wao wafanyabiashara wa mboga mboga nao wanalalamika kuwa kwanza upatikanaji wa mboga wenyewe ni mgumu kwani hulazimika kutembea umbali mrefu kuzifuata huko mashambani. Lakini pia wamelalamikia uhaba wa wateja kwani wakazi wengi hawapendi kula mboga za majani kutokana na sababu hizo za kwamba haziandaliwi katika mazingira masafi. Wengi wamesemakama vyanzo vya maji kama mito na mabwawa vingetunzwa katika hali ya usafi ingesaidia sana katika ulimaji wa bustani na hivyo wakazi wengi wangejenga tabia ya kula mboga za majani ambazo ni muhimu kwa afya zao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni