MGOGORO WA WAFANYABIASHARA SOKO LA NEWALA WAPATIWA UFUMBUZI WA MUDA
- ULIHUSU USHUSHAJI WA MIZIGO ENEO LA SOKO
- ULIPELEKEA WAFANYABIASHARA KUGOMA KWA SIKU MBILI
Mgogoro uliokuwa umeanza kuibuka katika soko kuu la wilaya ya Newala baina ya wafanyabiashara wa soko hilo kwa upande mmoja na Serikali kwa upande mwingine sasa umepatiwa ufumbuzi wa muda. Mgogoro huo ulianza pale mamlaka ya mji mdogo wa Newala ilipotoa agizo kwamba malori yote makubwa ya mizigo sasa hayataruhusiwa kushusha mizigo katika barabara zinazozunguka soko hilo ambalo lipo katikati ya mji. Sababu kubwa iliyotolewa ni ufinyu wa maeneo yenyewe ya kushushia hali ambayo inasabisha msongamano mkubwa na inaweza kusababisha hata ajali. Hivyo iliamriwa kwamba sasa magari yote makubwa yatashushwa eneo la pembeni ya stendi kuu ya mabasi yaendayo sehemu mbalimbali kutoka hapa wilayani ambapo ni zaidi ya kilometa mbili kutoka lilipo soko na baada ya hapo mizigo hiyo ibebwe na magari madogo mpaka sokoni.
Kitendo hicho hakikuwafurahisha wafanyabiashara wa soko hilo ambapo madai yao makubwa yalikuwa kwanza ni umbali ambao unasabisha kuongezeka kwa gharama na pia eneo lenyewe si salama na halina hata sehemu ya kuhifadhia mizigo. Walidai kuongezeka kwa gharama hizo za kufikisha mizigo kutapelekea wao kupandisha bei ya bidhaa na hivyo kumuathiri zaidi mnunuzi ambaye ni mwananchi wa kawaida.
![]() |
Kaimu mkuu wa Mkoa akiongea na wafanyabiashara |
Kaimu mkuu wa Mkoa huyo kwanza aliamua kwenda kutembelea eneo walilotengewa wafanyabiashara kwa ajili ya kushushia mizigo na kuahidi kutoa tamko ndani ya siku mbili. na kuanzia siku ya Tarehe 25 Desemba uamuzi umefikiwa kwamba sasa magari yote makubwa yatashushia mizigo yao eneo la Shirika la maendeleo la Newala (NEDECO)ambalo lipo kama mita mia mbili hivi kutoka sokoni huku ufumbuzi wa kudumu ukiendeela kutafutwa. Kwa mujibu wa diwani wa kata ya Mtonya Mheshimiwa Masoud Ismael Mbelenje tayari swala hilo limekwishaanza kutafutiwa ufumbuzi katika ngazi husika za wilaya.
![]() |
Biashara zikiendelea kama kawaida |
![]() |
Mizigo ikishushwa na kupakiwa kwenye magari madogo |
Kwa upande wa wananchi wa kawaida wengi wamefurahishwa na uamuzi wa kuendelea kufunguliwa kwa soko, kwani kwa siku mbili za tarehe 22 na 23 ambapo soko halikufunguliwa ilikuwa ni adha kubwa kwao katika kujipatia mahitaji yao ya kila siku.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni