Ijumaa, 26 Desemba 2014

MGOGORO WA WAFANYABIASHARA SOKO LA NEWALA

MGOGORO WA WAFANYABIASHARA SOKO LA NEWALA WAPATIWA UFUMBUZI WA MUDA

  • ULIHUSU USHUSHAJI WA MIZIGO ENEO LA SOKO
  • ULIPELEKEA WAFANYABIASHARA KUGOMA KWA SIKU MBILI
Mgogoro uliokuwa umeanza kuibuka katika soko kuu la wilaya ya Newala baina ya wafanyabiashara wa soko hilo kwa upande mmoja na Serikali kwa upande mwingine sasa umepatiwa ufumbuzi wa muda. Mgogoro huo ulianza pale  mamlaka ya mji mdogo wa Newala ilipotoa agizo kwamba malori yote makubwa ya mizigo sasa hayataruhusiwa kushusha mizigo katika barabara zinazozunguka soko hilo ambalo lipo katikati ya mji. Sababu kubwa iliyotolewa ni ufinyu wa maeneo yenyewe ya kushushia hali ambayo inasabisha msongamano mkubwa na inaweza kusababisha hata ajali. Hivyo iliamriwa kwamba sasa magari yote makubwa yatashushwa eneo la pembeni ya stendi kuu ya mabasi yaendayo sehemu mbalimbali kutoka hapa wilayani ambapo ni zaidi ya kilometa mbili kutoka lilipo soko na baada ya hapo mizigo hiyo ibebwe na magari madogo mpaka sokoni.

Kitendo hicho hakikuwafurahisha wafanyabiashara wa soko hilo ambapo madai yao makubwa yalikuwa kwanza ni umbali ambao unasabisha kuongezeka kwa gharama na pia eneo lenyewe si salama na halina hata sehemu ya kuhifadhia mizigo. Walidai kuongezeka kwa gharama hizo za kufikisha mizigo kutapelekea wao kupandisha bei ya bidhaa na hivyo kumuathiri zaidi mnunuzi ambaye ni mwananchi wa kawaida.

Kaimu mkuu wa Mkoa akiongea na wafanyabiashara
Mvutano huo ulipelekea wafanyabiashara wa soko hilo kuandika barua kwenda Halmashauri wakitoa mpaka tarehe 22 ya mwezi huu Desemba kushughulikia madai yao, lakini ilipofika tarehe hiyo huku wakiwa hawajapata majibu yoyote ndipo wakaamua kugoma kufungua biashara zao kwa siku mbili yaani tarehe 22 na 23 ya mwezi huu. Mgomo huo ulipelekea Serikali kuitisha kikao cha wafanyabiashara wote siku ya tarehe 23 mwezi huu na kuendeshwa Kaimu mkuu wa Wilaya ya Newala ambaye pia anakaimu nafasi ya mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa wilaya ya Tandahimba Mheshimiwa Ponsiano Damiami na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wafanyabiashara hao.Baada ya kikao hicho wafanyabiashara walifungua biashara zao kuanzia kesho yake yaani tarehe 24 na hivyo kuwawezesha watu kujipatia mahitaji yao ya kila siku ikiwemo maandalizi ya sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya.


Kaimu mkuu wa Mkoa huyo kwanza aliamua kwenda kutembelea eneo walilotengewa wafanyabiashara kwa ajili ya kushushia mizigo na kuahidi kutoa tamko ndani ya siku mbili. na kuanzia siku ya Tarehe 25 Desemba uamuzi umefikiwa kwamba sasa magari yote makubwa yatashushia mizigo yao eneo la Shirika la maendeleo la Newala (NEDECO)ambalo lipo kama mita mia mbili hivi kutoka sokoni huku ufumbuzi wa kudumu ukiendeela kutafutwa. Kwa mujibu wa diwani wa kata ya Mtonya Mheshimiwa Masoud Ismael Mbelenje tayari swala hilo limekwishaanza kutafutiwa ufumbuzi katika ngazi husika za wilaya.

Biashara zikiendelea kama kawaida
Uamuzi huo umeonekana kuwaridhisha kwa kiasi wafanyabiashara hao huku wakiwa wana matumaini ya kupata ufumbuzi wa kudumu. Bwana Hamis Namata ni muuzaji maarufu wa viungo vya chakula na madawa ya asili sokoni hapo anasema uamuzi huo umekuwa ni nafuu kwao kwani angalau sasa wanashusha mizigo karibu na maeneo ya biashara zao. Hata hivyo amezitaka mamlaka husika kuangalia jinsi ya kuboresha miundombinu ya eneo husika kwani hivi sasa hakuna hata sehemu ya kuhifadhia mizigo pindi inaposhushwa. Amesema hii itakuwa tatizo endapo mvua itaanza kunyesha na kupelekea uharibifu wa bidhaa kwani hakuna pa kuhifadhi, lakini alimaliza kwa kusema ana matumaini ufumbuzi wa kudumu utapatikana.

Mizigo ikishushwa na kupakiwa kwenye magari madogo
 Hivi sasa magari makubwa yameonekana yakishusha mizigo katika eneo hilo la NEDECO na maeneo mengine nje ya mji na kufanya barabara zinazolizunguka soko kuu kuonekana magari madogo maarufu huku kwa jina la vikeri (yaani carry) yakishusha mizigo, na hii kwa upande mwingine imekuwa ni faida kwa wenye magari madogo maana biashara imeongezeka sasa kwao tofauti nahapo nyuma magari makubwa yalipokuwayanashushia nje ya soko.

Kwa upande wa wananchi wa kawaida wengi wamefurahishwa na uamuzi wa kuendelea kufunguliwa kwa soko, kwani kwa siku mbili za tarehe 22 na 23 ambapo soko halikufunguliwa ilikuwa ni adha kubwa kwao katika kujipatia mahitaji yao ya kila siku.



Ijumaa, 17 Oktoba 2014

CHANGAMOTO YA UHABA WA MAJI NA KILIMO CHA MBOGA MBOGA DAR ES SALAAM

CHANGAMOTO YA UHABA WA MAJI NA KILIMO CHA MBOGA MBOGA DAR ES SALAAM

Tatizo la upatikanaji wa maji katika jiji la Dar Es Salaam limekuwa sugu sasa na kuwa kero kwa wakazi wengi wa jiji hili kubwa kuliko yote nchini. Wakati imekuwa ni shida kupata maji kwa matumizi muhimu ya kila siku kama vile kupikia, kunywa na kufanya usafi hali hii imekuwa kikwazo kikubwa kwa ukulima wa bustani  za mboga mboga kwenye jiji hili lenye takribani watu milioni tano. kwa sababu kilimo cha mboga kinahitaji maji mengi kwa ajili ya umwagiliaji hivyo tatizo hili la maji limefanya watu wengi kushindwa kujilimia mboga wenyewe na kutegemea kununua kwa wauzaji.

Maji yanayotumika kumwagilia bustani za mboga eneo la Mbezi Mwisho
Na kwa wakulima wanaojishughulisha na kilimo cha mboga mboga kilio kimekuwa ni hicho hicho cha ukosefu wa maji ya kumwagilia. Hali hii imepelekea watu kumwagilia kwa kutumia maji machafu yanayotiririka kwenye mifereji au yaliyotuama pembezoni mwa bustani zao hali ambayo imefanya watu wengi kutokuwa na imani na usalama wa mboga hizo. Abdallah Said ni mkulima wa eneo la mbezi mwisho anayelima mchicha, chinese  na aina nyingine ya mboga za majani, anasema wanalazimika kumwagilia kwa kutumia maji machafu kwa sababu ndio yanayopatikana hivyo hawana njia nyingine ya kufanya. Anaongeza kuwa ni kweli kuna baadhi ya watu ambao hawapendi kula mboga za majani kwa sababu ya maji machafu wanayotumia kumwagilia. Bwana Said anasema hali hii imefanya kutokuwa na wateja wengi na hivyo kuwa ngumu kwa wao kupata kipato cha kutosha kwa ajili ya kujikwamua na umaskini.

Bustani ya Mchicha
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa jiji hili walioongea na nurumpya wameonesha wasiwasi juu ya afya zo kutokana na kula mboga zinazolimwa katika mazingira machafu kama ilivyo maeneo mengi ya Dar Es Salaam. Wengi wa waliohojiwa wamesema wanakula kwa sababu tu hakuna namna nyingine huku wakimwomba Mungu awanusuru na madhara wanayoweza kuyapata kutokana na kula mboga zinazomwagiliwa na maji taka. Bi Sofia Mushi mkazi wa Kimara, Dar es Salaam amesema yeye kwa upande wake hana jinsi kwa sababu anajua mboga za majani ni muhimu kwa afya ya familia yake hivyo inambidi tu anunue bila kupenda. Lakini wakati bi Mushi akibainisha hayo mkazi mwingine Mwanaisha Shabani amesema yeye hununua mboga za maji kutokana na unafuu wa bei ukilinganisha na bei ya mboga nyingine kama nyama hivi. Anasema swala la kupata au kutokupata madhara kutokana na kula mboga hizo anamuachia Mungu wake.

Na japokuwa kuna wakati wakazi wengi wa Dar Es Salaam walipigia kelele swala la mboga za majani kumwagiliwa kwa kutumia maji taka bado imeoneakana hakuna ufumbuzi wa haraka wa tatizo lenyewe. kwani kama wanavyolalamika wakulima wenyewe tatizo kubwa ni upatikanaji wa maji, na sehemu kubwa zinazolimwa mboga hizi ni kwenye mabonde ambapo ndio kunapatikana maji ya mito. Na bahati mbaya sana ni kwamba mito yote ya jiji hili imejaa uchafu kupitiliza


Wafanyabiashara wa mboga za majani wakiwa sokoni
Kwa upande wao wafanyabiashara wa mboga mboga nao wanalalamika kuwa kwanza upatikanaji wa mboga wenyewe ni mgumu kwani hulazimika kutembea umbali mrefu kuzifuata huko mashambani. Lakini pia wamelalamikia uhaba wa wateja kwani wakazi wengi hawapendi kula mboga za majani kutokana na sababu hizo za kwamba haziandaliwi katika mazingira masafi. Wengi wamesemakama vyanzo vya maji kama mito na mabwawa vingetunzwa katika hali ya usafi ingesaidia sana katika ulimaji wa bustani na hivyo wakazi wengi wangejenga tabia ya kula mboga za majani ambazo ni muhimu kwa afya zao.

Ijumaa, 3 Oktoba 2014

WAKULIMA WANAWAKE WA MANANASI BAGAMOYO KUKAUSHA MANANASI KISASA KWA KUTUMIA JUA 

Wakulima wanawake wa mananasi kutoka katika kata za Kiwangwa na Fukayosi wilayani Bagamoyo wanatarajia kuanza kukausha mananasi kwa kutumia makaushio ya kisasa yanayotumia jua ambayo yamejengwa katika vijiji vya Kiwangwa kwa kata ya Kiwangwa na Mwavi kwa kata ya Fukayosi. Wanawake hao amabo wanaunda umoja unaoitwa UMOJA WA KUFUTA UMASKINI KATA YA KIWANGWA NA FUKAYOSI (UFUMA-KIFU) wamefanikiwa kupata makaushio hayo chini ya mradi wa KUONGEZA THAMANI YA ZAO LA NANASI KWA WAKULIMA WANAWAKE wilayani Bagamoyo, mradi unaofadhiliwa na kampuni ya FARM AFRICA ya nchini Uingereza na kuendeshwa na kampuni ya kitanzania ya DORT AFRICA yenye ofisi zake jijini Dar Es Salaam. 

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa kampuni ya DORT AFRICA, Assumpta Nalitolela makaushio hayo yaliyojengwa kwa gharama ya karibu shilingi milioni kumi na saba (17,000,000) kila moja yatasaidia katika uongezaji wa thamani ya zao la nanasi na hivyo kuongeza kipato kwa wanawake hao. Amebainisha kuwa kwa kuwa lengo la mradi huo ulioanza toka mwaka 2012 mi kuongeza kipato cha wanajamii, hivyo wameona kwa kukausha mananasi kwa kutumia jua maana yake ni kwamba sasa wataweza kuuza mananasi mabichi na yaliyokaushwa, na hii itaongeza kipato kwani sasa mkulima atakuwa na masoko mawili.

Kaushio la matunda linalotumia jua katika kijiji cha Kiwangwa



Naye mwenyekiti wa UFUMA-KIFU bi Farida Mrisho amesema wanategemea kuanza kukausha rasmi msimu huu wa mavuno ambao uko karibu kwani mananasi yameshaanza kuiva mashambani. Ameongeza kuwa kwa sasa bado wako kwenye mchakato wa kupata vibali kutoka TBS ili kuhakikisha wanauza bidhaa zenye ubora unaokubalika. 

Ingawa kuna njia nyingi za ukaushaji wa mboga na matunda lakini njia ya kutumia jua imekuwa ni rahisi zaidi kwani licha ya kuwa haiharibu mazingira lakini pia haihitaji nishati nyingine ya ziada kama vile umeme amabo ni gharama na si wa uhakika kwa nchi kama Tanzania.

Viongozi wa UFUMA-KIFU, kutoka kushoto Makamu Mwenyekiti Mtoro Idd, Mwenyekiti Farida Mrisho na Katibu Mwanahawa Mfikirwa